A great place to access the latest news and information.

Breaking

Post Top Ad

Your Ad Spot

Monday, May 21, 2018

Maagizo ya JPM baada ya kupokea taarifa ya uhakiki wa mali za CCM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCMDr. John Magufuli leo May 21, 2018 amepokea ripoti ya tume aliyoiunda kuhakiki mali za chama hicho, iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa tume hiyo Dr. Bashiru Kakurwakatika ofisi ndogo ya CCM Lumumba DSM.
Kamati hiyo imefanya kazi kwa miezi 5 ambapo imekusanya taarifa, imehakiki na kuchambua taarifa na nyaraka zenye maelezo kuhusu idadi, aina na hali ya mali zinazomilikiwa na kusimamiwa na chama, imeangalia vyanzo vya udhaifu wa mifumo na taratibu za usimamizi wa mali.
Mwenyekiti wa tume hiyo Dr. Kakurwa amesema uhakiki huo umefanyika kwa kutembelea maeneo yenye mali za chama, kuwahoji watu mbalimbali wakiwemo viongozi waliohusishwa na mali zilizokuwa zikihakikiwa, upitiaji wa nyaraka na kufuatilia uhalisia katika ofisi za mamlaka husika, kufanya uchambuzi wa taarifa na kutoa mapendekezo.
Ameongeza kuwa uhakiki huo umefanyika katika mali za chama zilizo chini ya baraza kuu, jumuiya za chama na kampuni za chama.
Katika ripoti hiyo Dr. Kakurwa amesema tume imebaini uwepo wa upotevu mkubwa wa mali za chama uliosababishwa na mikataba mibaya, ubadhilifu, wizi, usimamizi mbaya wa mali, utapeli na ukosefu wa maadili katika uendeshaji wa miradi ya chama. 
Dr. Magufuli ameipongeza tume hiyo kwa kazi kubwa iliyoifanya na amesema ripoti hiyo itawasilishwa katika vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM kwa ajili ya kufanyiwa uamuzi.
“Nilipokuwa nateua tume hii nilikuwa najua ugumu wa kazi, nilikuwa najua kuwa mtapata shida kwenda kuwahoji watu licha ya kwamba niliwapa uhuru wa kumhoji mtu yeyote na mmefanya kazi nzuri sana, kilichobaki sasa ni kuifanyia kazi”amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amewaagiza wajumbe wa sekretarieti ya CCM waliohudhuria wakati wa uwasilishwaji wa ripoti hiyo kuanza kufanyia kazi baadhi ya mambo yaliyo ndani ya uwezo wao na kwamba masuala mengine yataamuliwa na vikao vikuu vya chama.
Kabla ya kuondoka katika ofisi ndogo za CCM Lumumba, Dr. Magufuli amesalimiana na wananchi waliokuwa nje ya ofisi hiyo na kuwahakikishia kuwa CCM imeamua kuhakiki mali zake ili kukiwezesha chama hicho kulinda mali zake na kunufaika na mali hizo.
Rais Magufuli amesisitiza kuwa CCM imeamua kuchukua hatua hiyo ikiwa ni utekelezaji wa dhamira yake ya kupiga vita rushwa na ufisadi na amewaeleza kuwa tume ya Dr. Kakurwa imefanya kazi nzuri.
“Huwezi ukaanza kupiga vita rushwa na ufisadi ndani ya Serikali wakati chama kina rushwa na ufisadi, chama nacho tunataka tukisafishe, mambo ya rushwa na ufisadi yaishe ili Tanzania iende vizuri,” Rais Magufuli
“Ndio maana tumeunda tume ya Dkt. Bashiru Ally, imefanya kazi nzuri sana, na ripoti hii tutaipeleka Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ndani ya mwezi huu ili tuijadili na viongozi watoe maelekezo” amesisitiza Rais Magufuli.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages