A great place to access the latest news and information.

Breaking

Post Top Ad

Your Ad Spot

Saturday, May 26, 2018

Dcp Mkumbo Awaaga Askari, Amkaribisha Rpc Mpya

Na Rashid Nchimbi Arusha
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo leo hii mchana amewaaga Maofisa, Wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali katika kikao kilichofanyika Bwalo la Maafisa wa Polisi lililopo jijini hapa.

Akizungumza na askari hao Naibu Kamishna Mkumbo ambaye amehamishiwa Makao Makuu ya Jeshi hilo, aliwashukuru askari wote wa mkoa huu kwa kushirikiana naye vizuri katika utendaji wa kazi hali ambayo ilisaidia kwa kiasi kikubwa kudumisha usalama  kwa kipindi chote alichokaa hapa.

Naibu Kamishna Mkumbo ambaye amefanya kazi mkoani hapa kwa takriba miaka miwili na miezi miwili alisema kwamba mafanikio ya kazi za kijeshi msingi wake mkubwa ni nidhamu na kufanya kazi kwa weledi.

Aliongeza kwa kusema kwamba, endapo askari wa mkoa wa Arusha wataendelea kudumisha nidhamu na kutoa huduma iliyo bora kwa wananchi basi ni wazi wananchi hao wataendelea kuliunga mkono Jeshi hilo kwa hali na mali.

Aliwataka askari hao kuendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa Kamanda mpya hali ambayo itasaidia kuzidi kuimarisha usalama wa mkoa na kuendelea kuwa kivutio kwa watalii na wawekezaji wa sekta nyingine.

Kwa upande wake Kamanda mpya wa mkoa huu Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng’anzi alisema kwamba, ataendeleza yale mema yaliyofanywa na mtangulizi wake na kuboresha zaidi pale ambapo panahitajika kufanya hivyo ili kuweza kuzidi kuimarisha usalama wa mkoa huu.

Alisema ili kufanikisha utendaji bora, askari anatakiwa afanye kazi kwa weledi, uaminifu na uadilifu, atoe huduma bora kwa mwananchi lakini pia alilisitiza nidhamu.

“Kama hakuna nidhamu basi hakuna Jeshi na ningependa tuishi kama familia moja hali ambayo itasaidia kumshinda adui”. Alisisitiza Kamanda Ng’anzi.

Katika kipindi chake cha uongozi mkoani hapa Naibu Kamishna Mkumbo kwa kushirikiana na askari aliweza kupunguza matukio ya uhalifu; ambapo matukio ya uhalifu yaliyoripotiwa kwa mwaka  2016 yalipungua kwa 6.8% ikilinganishwa na mwaka 2015 na takwimu za matukio ya uhalifu kwa mwaka 2017 yalipungua zaidi kwa 17.9% ambapo kati ya hayo matukio ya uvunjaji yalishuka toka 604 mwaka 2016 hadi kufikia 294.

Mbali na hayo Naibu Kamishna Mkumbo alikuwa anawaongoza askari katika mazoezi ya riadha ambapo kila Jumamosi alikuwa akikimbia kilomita 10 hadi 15 hali ambayo ilizidi kuwatia moyo wa kufanya mazoezi binafsi askari wa mkoa wa Arusha lakini pia aliweza kuwahamasisha askari kushirikia hatua nusu marathoni mashindano mbalimbali ya riadha kama vile Kili Marathon na kadhalika.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages