A great place to access the latest news and information.

Breaking

Post Top Ad

Your Ad Spot

Monday, May 7, 2018

Bodi ya mikopo kuanza kupokea maombi ya Mikopo mwezi huu


Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inapenda kuwataarifu wananchi kuwa inatarajia kuanza kupokea maombi ya mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2018/2019 kuanzia wiki ya kwanza ya mwezi Mei, 2018 baada ya kukamilishwa kwa maboresho makubwa ya mfumo wa uombaji kwa njia ya mtandao.

Maboresho ya mfumo wa maombi
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru amesema katika taarifa yake ya Aprili 17, 2018 kuwa maombi yote yatapokelewa kwa njia ya mtandao (www.olas.heslb.go.tz) ambao umefanyiwa maboresho na Kituo cha Kompyuta cha Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UCC-UDSM).

Aidha, Bw. Badru amesema dirisha hilo litafunguliwa sambamba na kutangazwa kwa mwongozo wa kina utakaotoa utaratibu wa kuwasilisha maombi, tarehe ya mwisho ya kuwasilisha maombi, sifa na vigezo vitakavyotumika katika kuchambua na kutoa mikopo kwa mwaka ujao wa masomo unaotarajiwa kuanza mwezi Oktoba, 2018.

“Tunawasihi wale wote wanaotarajia kuomba mkopo wa elimu ya juu kusoma kwa makini mwongozo tutakaoutoa kwa vyombo vya habari na tovuti mwanzoni mwa mwezi Mei, 2018 na kuuzingatia,” amesema Bw. Badru.

Bw. Badru amefafanua kuwa wito wa Bodi ya Mikopo umetolewa kutokana na uzoefu wa miaka iliyopita ambapo waombaji wa mikopo waliwasilisha maombi yao bila kuzingatia mwongozo uliotolewa na kusababisha baadhi ya wanafunzi kukosa mikopo.

“Mwaka jana, kwa mfano, zaidi ya waombaji 10,027 kati ya waombaji zaidi ya 61,000 hawakuambatisha nyaraka muhimu kama vyeti vya kuzaliwa au hata vile vya vifo vilivyothibitishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kama tulivyoelekeza,” amesema.

Nyaraka muhimu zinazohitajika
Nyaraka nyingine muhimu ambazo waombaji mikopo wanapaswa kuziandaa ni pamoja na nakala za vyeti vya kitaaluma za kidato cha nne, sita na stashahada ambazo zimethibitishwa na Kamishna wa Viapo yaani Wakili au Hakimu.

Aidha, wanafunzi waombaji wenye ulemavu au wenye wazazi wenye ulemavu wanapaswa kuwa na barua zinazothibitisha ulemavu huo kutoka kwa Mganga Mkuu wa Mkoa, Wilaya au Kituo cha Afya cha Serikali;

Bw. Badru ameongeza kuwa wanafunzi ambao walifadhiliwa katika masomo yao ya Sekondari au Stashahada (Diploma) wawe na barua za uthibitisho wa udhamini huo kutoka katika taasisi zilizogharamia masomo yao.

Maafisa wa HESLB kutoa elimu mikoani
Katika hatua nyingine, Bw. Badru amesema mwaka huu maafisa wa Bodi ya Mikopo watatembelea mikoa mbalimbali ili kukutana na waombaji mikopo kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu taratibu sahihi za kuwasilisha maombi yao ya mikopo kwa njia ya mtandao. Ratiba na maeneo itakapofanyia mikutano hiyo itatangazwa mwanzoni mwa mwezi Mei, 2018.

HESLB ilianza kazi rasmi mwaka 2005 ili, pamoja na majukumu mengine, kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa watanzania wahitaji na wenye sifa na kukusanya mikopo iliyoiva ambayo ilitolewa na Serikali tangu mwaka 1994/1995.

Imetolewa na:
Abdul-Razaq Badru
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
DAR ES SALAAM
Kwa ufafanuzi: +255 (0) 757 500800

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages