BAADA ya utata kugubika kifo cha mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Afya ya Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Marcus Edward Kahitwa, Risasi Mchanganyiko limefuatilia tukio hilo na sasa linakujuza mwanzo hadi mwisho.

Mwili wa mwanafunzi huyo, uligundulika Mei 19, mwaka huu katika chumba namba 65 kilichopo katika Hosteli ya Kagera alipokuwa akiishi peke yake.

Mara baada ya kutokea kwa tukio hilo, baadhi ya wanafunzi walionesha kushtushwa na mazingira ya kifo chake hivyo kila mtu kuzungumza lake.
Utata zaidi ulijitokeza kutokana na jinsi mwili wa mwanafunzi huyo alivyokaa kwa takriban siku mbili bila kugundulika na wanafunzi wenzake waliopo katika hosteli hiyo.

Akizungumza na Gazeti letu la Risasi, ofisa uhusiano wa chuo hicho, Hellen Mtui alisema kuwa mwili wa Marcus ulikutwa chumbani kwake ukiwa kitandani Jumamosi iliyopita baada ya kuonekana mara ya mwisho siku ya Alhamisi.

“Ilikuwa Alhamisi iliyopita alikuwa na wenzie kama kawaida na akawaambia kwamba huenda angekwenda kwa ndugu zake, lakini ilipofika Ijumaa hakuonekana chuoni kitu ambacho kiliwafanya wanafunzi wenzake wahisi kuwa huenda atakuwa amelala.


“Lakini ilipofika Jumamosi wanafunzi wenzake wakaona mlango wake umefungwa muda mrefu wakawa na wasiwasi wakaamua kwenda kituo cha polisi ambacho kipo hapahapa Muhimbili na kuripoti, baada ya hapo polisi wakaja na kuvunja mlango kwa sababu alikuwa amefunga mlango wake kwa ndani lakini walikuta amelala kitandani akiwa amefariki,” alisema Hellen.

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko juzi wakati wa ibada ya kuaga mwili wa Marcus, kaimu makamu mkuu wa chuo hicho, Prof. Appolinary Kamuhabwa alisema, uchunguzi wa awali unaonesha kuwa, kifo cha Marcus kimetokana na ukosefu wa hewa katika mfumo wa hewa.
Alisema inaonekana marehemu alicheua chakula kikaingia kwenye mfumo wa hewa na kumsababishia ashindwe kupumua vizuri hivyo kupoteza maisha.




Makamu huyo mkuu alisema hata hivyo, madaktari wanaendelea na uchunguzi zaidi na wakibaini zaidi kuhusu kifo hicho, watatoa ripoti.
“Kama mwanafunzi amefariki chumbani lazima mwili ufanyiwe uchunguzi lakini vipimo vya awali vinaonyesha marehemu amefariki kwa kukosa hewa kwa sababu inaonekana Marcus alicheua chakula na kikaingia kwenye mfumo wa hewa kwa hiyo uchunguzi bado unaendelea,” alisema Prof Kamuhabwa.
Akizungumzia wasifu wa marehemu, baba mdogo wa marehemu Marcus, Mhandisi Kahitwa Bishaija alisema Marcus alizaliwa jijini Mbeya na kupata elimu yake huko na baba yake mzazi alishafariki.

Alisema licha ya kuzaliwa jijini Mbeya lakini Marcus asili yake ni wilayani Muleba, Mkoa wa Kagera na kama familia, wamepata pigo kubwa sana kwa sababu kijana huyo alikuwa anaelekea kumaliza masomo yake.

“Kwa kweli ni pigo kubwa maana tuliamini sasa anakwenda kuwa msaada kwa familia lakini ndiyo hivyo ametutoka, tunamshukuru Mungu maana kazi yake haina makosa,” alisema baba mdogo huyo wa marehemu.

Mmoja wa marafiki wa marehemu ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, alisema kama mwanachuo mwenzao, wamepata pigo kubwa sana kwa sababu marehemu alikuwa msaada mkubwa sana katika masomo yao na alikuwa akimsadia mtu yeyote bila kubagua.
“Yaani kwa kweli hakuwa mtu wa kinyongo, alikuwa akijitoa hata kwa wanafunzi ambao si wa darasa lake kwa kweli kifo chake kimetuliza wengi,” alisema rafiki huyo wa marehemu.
Mwili wa marehemu Marcus uliagwa juzi na wanafunzi wenzake pamoja na walimu katika Ukumbi wa Chuo cha Muhas na kusafirishwa kijijini kwao Bugarama, wilayani Muleba, Kagera kwa ajili ya mazishi.
Marehemu Marcus alizaliwa Julai 7, 1995 na kufariki dunia Mei 18, 2018.
MUNGU AILAZE ROHO YAKE MAHALI PEMA PEPONI AMINA.
STORI: Neema Adrian, Risasi Mchanganyiko