Wananchi wa kata ya Ilala tawi la msimbazi mivinjeni wameiomba serikali kuwasaidia kutatua kero za miundombinu zinazowakabili ikiwemo ujenzi wa barabara na mifereji ya kupitishia maji ili waweza kuwafikisha wagonjwa hospitalini.
Hayo yamejiri kwenye mwendelezo wa ziara ya chama Cha mapinduzi CCM wilaya ya Ilala ya kutembea kata na mashina yake ambapo Mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo Abdul-azizi Ubaya Chuma amesema kuwa kero hizo watahakikisha zinatatuliwa na viongozi wa maeneo hayo akiwemo mbunge na diwani wake.
Aidha wananchi hao wameiomba serikali pia kuwasaidia kupata ufumbuzi wa upatikanaji wa mikopo haswa kwa kinamama na vijana ili waweza kuendeleza biashara zao na kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande mwingine wakazi wa tawi la shauri moyo wamekiomba chama Cha mapinduzi kuwasaidia kutatua kero wanayokumbana nayo ya kujaa matope katika soko la ilala na baadhi ya mifereji katika eneo hilo kujaa maji.
Akizungumza katika tawi hilo Katibu Muenezi CCM wilaya ya Ilala Said Side amewataka wakazi hao kuwa wavumilivu kwani Manispaa ya Ilala imeandaa mchakato wa kuboresha masoko yote yaliyopo ndani ya wilaya hiyo.
" Tayari soko la kisutu liko kwenye marekebisho na jitihada za serikali zipo za kutosha kwani tumeongea na Diwani wa eneo hili na fedha za kurekebisha masoko mengine tayari zishatengwa", amesema side.
Hata hivyo katika ziara hiyo viongozi wa CCM wilaya ya Ilala walifanikiwa pia kutembelea katika kata ya upanga mashariki na upanga magharibi .



No comments:
Post a Comment