A great place to access the latest news and information.

Breaking

Post Top Ad

Your Ad Spot

Tuesday, April 3, 2018

Chereko Chereko Bombadier ya tatu yawasili nchini.


NDEGE aina ya Bombardier Dash 8 Q400, ambayo ilikuwa imezuiliwa Canada kwa amri ya mahakama na ambayo Rais John Magufuli alimuandikia barua waziri mkuu wa nchi hiyo na kumtuma mwanasheria mkuu wa serikali kuifuatilia mwishoni mwa mwaka jana, iliwasili jana nchini kukiwa na chereko chereko.

Katika chereko chereko hizo, Rais Magufuli alitoa agizo kwa mamlaka kuruhusu wananchi waliofika katika hafla hiyo kuingia ndani ya Bombadier katika makundi ya watu 76 kwa mara moja lakini mpaka waishe, ili kwenda kupiga picha wakiwa wamekaa humo.

Ni mara ya kwanza katika historia ya ununuzi wa ndege nchini kwa wananchi kuruhusiwa kuingia ndani ya chombo hicho kwa ajili ya kukijaribisha.

Kuwasili kwa Bombadier hiyo kunafanya jumla ya ndege tatu za aina hiyo zilizonunuliwa na serikali kufika na kubakiza ndege kubwa nyingine tatu ambazo mbili ni Bombardier CS300 kutoka Canada pia na Boeing 787-8 Dreamliner kutoka Marekani.

Ndege hiyo ilitua uwanjani hapo saa 11:07 jioni na kupigiwa saluti ya maji, kama ilivyo utamaduni, kwa magari mawili ya zimamoto na baadaye Rais kukata utepe na kisha kuingia ndani, Baada ya kutoka ndipo Rais Magufuli alitoa ruhusa kwa wananchi nao kupewa fursa hiyo.

Akizungumza katika uzinduzi wa Uwanja wa Ndege wa Bukoba Novemba 6, mwaka jana, Rais Magufuli alisema amemuandikia barua waziri mkuu wa nchi hiyo kujua kwa nini "ndege yetu" imekaa zaidi ya miezi sita na kwamba Watanzania wamechoka kusubiri.

Aidha, Rais Magufuli alisema katika halfa hiyo kuwa alimtuma nchini humo Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa wakati huo, George Masaju, kushughulikia kisheria.

Katika mkutano huo, Rais Magufuli aliwahakikishia Watanzania kuwa ndege zote sita zilizonunuliwa na Serikali kwa ajili ya Shirika la Ndege la ATCL zitakuja, na sasa Bombardier Dash 8 Q400 ya tatu imetua pia.  

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages