MOZE WAKATI WA UHAI WAKE AKIWA NA MKEWE, LEE AMBAYE NI MSANII WA KUNDI MAARUFU LA ZAMANI LA BLUE3
ENTEBBE, Uganda
MWANAMUZIKI wa Uganda, Moze Radio amefariki dunia baada ya kulazwa katika Hopitali ya Case kwa siku kumi.
Msanii huyo alifikishwa hospitalini hapo baada ya kushambuliwa na baunsa wa ukumbi wa muziki baada ya kutokea mzozo jijini Entebbe.
Moze pamoja na Weasel waliunda Kundi la GoodLife ambapo walitamba na nyimbo nyingi. Wiki mbili zilizopita wawili hao walikuwa kwenye Ukumbi wa De Bar ambapo kuna taarifa nyingi tofauti zinatoka juu ya chanzo cha ugomvi uliotokea.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa Moze alipofika ukumbini humo akaungana na marafiki zake, usiku majira ya saa tisa akaonana na mmiliki wa klabu hiyo aliyetajwa kwa jina la George Egesa.
Inaelezwa Moze alimtolea lugha kali mmiliki huyo baada ya kuwa ‘amekolea’ kwa kinywaji, akamwambia ‘amefulia’ na hana fedha hata ya kumnunulia mvinyo aina ya Johnnie Walker.
Baada ya kuona hivyo, Egessa akaagiza mhudumu ampatie Moze mvinyo huo jambo ambalo lilitekelezwa, baada ya kukabidhiwa mvinyo, Moze akaumwaga juu ya meza badala ya kuunywa, kitendo ambacho kilimkasirisha mmiliki ambaye aliagiza baunsa wake amtoe nje Moze.
Hapo ndipo kukatokea vurugu na baadaye baunsa huyo alifanikiwa kumtoa Moze lakini muda mfupi baadaye akakutwa amelala chini nje ya ukumbi huo hajitambui.
Alipokimbizwa hospitali ikagundulika amepata mtikisiko wa ubongo. Rais wa Uganda, Yowel Museven alikuwa mmoja waliojitokeza kusaidia matibabu ambapo alitoa Sh milioni 30 kuchangia matibabu lakini siku moja baadaye ambayo ni jana Moze akakata kauli.
Mmiliki wa klabu na baunsa aliyehusika wote wapo kwenye mikono ya sheria hadi habari hii ilipokuwa ikiandikwa, jana jioni.
Kabla ya kuwa staa, Moze aliwahi kuwa dereva wa msanii Jose Chameleone, kisha akawa msaidizi wake wa kuimba jukwaani na mwisho kuwa mwanamuziki kamili ambapo alishirikiana vizuri na Weasel ambaye ni mdogo wa Chameleone.
Jina kamili ya Moze ni Moses Nakintije Ssekibogo, alitimiza umri wa miaka 33, Jumapili iliyopita akiwa kitandani.
No comments:
Post a Comment