Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa ameagiza kukamatwa kwa meneja wa Benki ya NMB, tawi la Masasi na kuwekwa chini ya ulinzi ili ufanyike uchunguzi wa sababu za baadhi ya wakulima kutolipwa fedha zao zaidi ya Sh3 bilioni.
Agizo hilo limetolewa jana Ijumaa Februari 23, 2018 baada ya meneja huyo kushindwa kuhamisha fedha za wakulima kutoka benki hiyo kwenda CRDB, huku akikopesha chama msingi kiasi cha Sh300 milioni bila chama kuomba ikiwa ni pamoja na muamala wa Sh45 milioni kulipwa mara 11 kwa siku moja.
Wengine walioagizwa kukamatwa ni pamoja na baadhi ya viongozi wa Amcos ambao waliwalipa wakulima mara mbili na kusabisha baadhi yao kudai malipo yao, wakiwemo waliopokea fedha hizo mara mbili.
Hatua hiyo imekuja baada ya Byakanwa kuagiza kuundwa kwa tume ili kuchunguza madai ya baadhi ya wakulima kutolipwa fedha za msimu wa mwaka 2016/17 na 2017/18.
Akisoma taarifa ya tume, Mwenyekiti wake, Remidius Bantulaki ameeleza sababu iliyochangia kucheleweshwa kwa malipo ni pamoja na NMB kuchelewa kutoa taarifa za vyama ambavyo miamala yake haijakamilika yenye thamani ya Sh400 milioni na mpaka tume inaandaa taarifa zilikuwa hazijarudishwa kwenye vyama vya ushirka.
“Mfano Chama cha Msingi Namalenga waliomba taarifa Desemba 6, 2017, lakini wamekuja kupatiwa yenye thamani ya Sh 12.4 milioni Februari 17, 2018,” alisema.
“Jambo lingine benki hiyo inachelewa kuhamisha fedha kwenda benki nyingine ili kulipa wakulima wanaotumia benki tofauti na wao,” amesema.
“Novemba 17, 2017 Chama cha Chimana kiliandika hundi ya Sh 45.5 milioni kwenda CRDB mpaka tarehe 12, hiyo fedha ilikuwa haipo kwenye akaunti ya chama wala kufika kwenye akaunti ya CRDB na wakulima walikuwa bado wanadai.”
Hata hivyo, ameeleza wamegundua baadhi ya vyama vya ushirika vimewalipa wakulima mara mbili na hivyo kuwalazimu ambao hawajalipwa kusubiri mpaka waliolipwa mara mbili kurudisha fedha.
“Kwenye Chama cha Nanjota Amcos mnada wa saba uliokuwa na kiasi cha Sh31.4 milioni uliokuwa na jumla ya wakulima 12, kuna wakulima wamelipwa mara mbili kwa hiyo wengine wanasubiri wao watakaporudisha fedha ndipo walipwe,” amesema.
Amesema tume hiyo imegundua benki ya NMB kutoa fedha kwenye akaunti ya chama mara mbili kinyume na taratibu.
“Chama cha Chimane Amcos iliyoandika hundi ya Sh45.5 milioni yenye namba 00040, Novemba 17 ilitolewa kwenye akaunti ya chama Novemba 18 2017, lakini kiasi hicho hicho kikatolewa tena Novemba 30, 2017 na kufanya fedha iliyotolewa kwa wiki moja kuwa Sh91.1 milioni na hiyo fedha haikufika kwenye akaunti ya CRDB wala kurudi kwenye akaunti ya chama.”
Baada ya taarifa hiyo, Byakanwa amekubaliana na mapendekezo yote ya tume na kutoa maagizo ya kukamatwa kwa watuhumiwa
No comments:
Post a Comment