Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wengine wachama hicho wameachiwa kwa dhamana baada ya kuhojiwa Kituo Kikuu cha Polisi tangu saa 6:50 mchana
Viongozi hao walifika kituoni hapo leo Jumanne Februari 27, 2018 na kuachiwa saa 1:02 usiku, kuitikia wito wa polisi.
Walikwenda kituoni hapo baada ya Mbowe kumaliza mkutano wake na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho yaliyopo mtaa wa Ufipa, Kinondoni.
Mmoja wa mawakili wa viongozi hao, Frederick Kihwelo ameileza MCL Digital leo kuwa wote wameachiwa kwa dhamana kwa kutakiwa kuwa na mdhamini mmoja na kutakiwa kuripoti tena kituoni hapo Machi 5, 2018 saa 1 asubuhi.
Amesema viongozi hao walianza kuhojiwa saa 8:30 mchana, baada ya kufanya mazungumzo ya tuhuma zinazowakabili.
Februari 20, 2018 Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam iliagiza kukamatwa viongozi saba waandamizi wa Chadema akiwamo Mbowe.
Wito huo ulikuja siku chache baada ya tukio la kuuawa kwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.
Akwilina aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Kinondoni jijini Dar es Salaam wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakienda ofisi za mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni kudai viapo kwa mawakala wao.
Viongozi wengine waliohojiwa sambamba na Mbowe ni naibu makatibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar).
Pia, wamo mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee; mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, John Heche na Esther Matiko ambaye ni mweka hazina wa Bawacha.
Mdee, Matiko, Heche na Mnyika walisharipoti awali na walitakiwa kurejea kituoni leo. Viongozi wengine waliwakilishwa na wanasheria.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji hakwenda polisi kwa kuwa yupo nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment