Serikali
imezindua mkakati unaolenga kutokomeza uvuvi haramu kwa kuanzisha operesheni ya
kutumia ndege maalumu itakayofanya doria katika eneo la bahari kuu.
Akizungumza
wakati wa kuzindua safari ya ndege ya kutoka nchini Mauritius iliyotua hapa
nchini, kwa mara ya kwanza kwa ajili ya kufanya doria ya majini, Naibu Waziri
wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega alisema lengo ni kudhibiti uvuvi
haramu katika eneo la bahari kuu.
Alisema
Serikali ya awamu ya tano imejipambanua juu ya ulinzi wa rasilimali za nchi,
ikiwamo meli ya uhakika ya majini, licha ya kukumbwa na dhoruba kubwa.
Amesema kutokana
na hali hiyo ndiyo maana wameunganisha nguvu kwa pamoja kati yao na Ukanda wa
nchi za Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi kudhibiti uvuvi haramu kwa njia
zote.
“Tunaruhusu
ndege ya doria leo, ili kuongezea nguvu njia za kudhibiti wavuvi haramu,
tulianza kwa njia ya bahari na sasa ni kwa njia ya anga.
“Changamoto
ya uvuvi haramu ni kubwa, mtu anapiga bomu kwenye matumbawe anafanya uharibifu
ambao kuyatengeneza tena yanachukua zaidi ya miaka 100, huku yeye akiharibu kwa
dakika tano, ” alisema Ulega.
Ulega
alisema uharibifu huo ndiyo unachangia kuwatia umasikini wavuvi wengi kwa
sababu siyo rahisi kupata samaki karibuni na kulazimika kwenda mbali ambako
siyo rahisi kufika bila kuwa na vyombo maalumu.
Kwa upande
wa Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar Hamad Rashid alisema atashauriana na marais wa pande zote mbili
kuangalia namna ya kurudisha Shirika la Uvuvi Tanzania (Tafico) na Shirika la
Uvuvi Zanzibar (Zafico).
Alisema
mashirika hayo yakifanya kazi kwa kushirikiana wananchi watapata fursa ya
kufurahia matunda yatokanayo na utajiri uliomo baharini.
“Katika
mwendelezo wa kupambana na uvuvi haramu na kulinda bahari ya Hindi Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar ilifanya mazungumzo ya kuingia ubia na Serikali ya China na
tayari kuna meli 10 zinafanya doria.
“Serikali
pia imeagiza boti 500 watakazopewa wavuvi ili wazitumie kuvua kisasa, pia
inasimamia ujenzi wa soko la samaki la kisasa na namna bora ya kuhifadhi samaki
awe katika hali yake ile ile hadi anamfikia mlaji, ” alisema Rashid.
Alisema
uvuvi haramu siyo tu janga kwa kuondoa rasilimali za bahari, pia ukiachwa
uendelee unaweza kuwa chanzo cha biashara nyingine haramu ikiwamo usafirishaji
wa watu, biashara ya dawa za kulevya na utakatishaji fedha.
Nae Katibu
mkuu Uvuvi Dk Yohana Budeba alisema ndege hiyo itafanya doria ya anga kwa siku
nne.
Kwa upande
wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya kusimamia uvuvi wa bahari kuu Hosea
Mbilinyi alisema ndege hiyo licha ya kuzunguka angani ikifanya doria, ina uwezo
wa kupiga picha na kueleza kinachoendelea.
Alisema
doria hiyo ni ya kikanda ambayo inahusisha nchi nane zikiwamo Tanzania Kenya,
Msumbiji, Ushelisheli, Reunion, Comoro, Mauritius na Madagascar.
Naibu
Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Abdallah Ulega akizungumza na
waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya operesheni ya kutumia ndege
maalumu itakayofanya doria katika eneo la bahari kuu kudhibiti uvuvi
haramu, leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Waziri wa Kilimo, Maliasili,
Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Hamad Rashid Mohamed.
Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Abdallah Ulega akishuka
kwenye ndege maalumu itakayofanya doria katika eneo la bahari kuu
kudhibiti uvuvi haramu mara baada ya kuikagua ndani.
Waziri
wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Hamad Rashid
Mohamed na Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Abdallah Ulega
pamoja na viongozi mbalimbali wakiangalia ndege maalumu ya doria katika
eneo la bahari kuu kudhibiti uvuvi haramu.
Waziri
wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Hamad Rashid
Mohamed naNaibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,Abdallah Ulega na
viongozi mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja
No comments:
Post a Comment