Tukielekea miaka miwili tangu kuapishwa kwa Rais John Pombe Magufuli kuwa Rais wa Awamu Ya Tano wa Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania ni wajibu wa kila Mtanzania mwenye kiu ya maendeleo na mzalendo kwa nchi yake kuunga mkono juhudi za Rais ili kuifikia Tanzania ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Nakumbuka hotuba yake ya kwanza baada ya kula kiapo cha kulitumikia Taifa hili aliyoitoa katika shughuli za kuapishwa uwanja wa Uhuru jijini Dar Es Salaam, Novemba 5, mwaka 2015 ambayo ilibeba maneno yenye busara, hekima na yenye hamasa ya kuleta maendeleo ya nchi yetu.
“Nchi yetu ni kubwa kuliko vyama vyetu vya siasa, mapenzi yetu na matakwa yetu.Uchaguzi Mkuu sasa umekwisha sote tushikamane kama watu wa Taifa moja kuijenga nchi yetu kwa kuweka itikadi na vyama vyetu pembeni”,alisema Rais Magufuli.
Ni wazi maendeleo ya nchi hayana dini, kabila, itikadi au chama bali yana undugu na uzalendo, ushirikiano, umoja, kufanya kazi kwa bidii na amani baina ya wananchi na serikali kwa ujumla.
Hivyo basi, tunawajibu wa kushikamana kama watoto wa baba mmoja na kufanya kazi kwa bidii na kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli kwa vitendo ili tuweze kuifikisha Nchi kwenye uchumi wa kati utakaotuwezesha kupambana na maadui wakubwa watatu ambao ni Maradhi, Ujinga na Umaskini badala ya kukaa vijiweni kujadili mambo yasiyo na tija kwa maendeleo yetu.
Aidha, hivi karibuni tumeshuhudia Taasisi, Mashirika,Viongozi mbalimbali wa dini na serikali na watu mbalimbali wakituma salamu za pongezi kwa Rais Magufuli kwa juhudi na utendaji kazi wake. Lakini je?,tumewahi kujiuliza pongezi hizi na za maneno tu au wanashiriki kwa vitendo?
Sina maana kuwa, kumpongeza Rais ni vibaya au uovu,ni jambo jema lakini ingekua vyema zaidi kama pongezi zingeambatana na vitendo kwani “maneno bila vitendo si kitu” ndio maana Serikali Awamu Ya Tano inaongozwa na kaulimbiu ya “HAPA KAZI TU” kwa lengo la kuhamasisha Watanzania kufanyakazi kwa bidiii badala ya kusubiri serikali kuwafanyia kila kitu.Kauli mbiu hii imekua ikitumika pia nchi mbalimbali duniani ili kuhamasishana katika kufanyakazi na kujiletea maendeleo.
Maneno ya Rais Magufuli alipohutubia Bunge la Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania kwa mara ya Kwanza yanaishi na kutekelezwa kwa vitendo katika Serikali ya Awamu ya Tano hadi kwa wananchi wenye kupenda maendeleo .
“Kila mmoja wetu afanye kazi, awe shambani, ofisini, kiwandani, sokoni, kwenye bustani na kadhalika badala ya kupoteza muda vijiweni”, alisema Rais Magufuli.
Ni wazi kuwa , Rais Magufuli amekuwa kiongozi anayeisimamia na kutekeleza kauli mbiu ya Serikali yake kikamilifu tangu aingie madarakani kwa kuwajibika ipasavyo katika kuhakikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo imekua na manufaa makubwa kwa wananchi na Serikali kwa ujumla.
Hivi karibuni, tumeshudia Mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda mpaka kwenye bandari ya Tanga kwasababu ni moja ya mradi mkubwa ambao nchi imetekeleza na utakaobadilisha maisha ya watanzania takribani elfu 30 kwa wakati mmoja. Pia, kuinufaisha Serikali kupitia kodi na utengenezaji wa ajira kwa wananchi wake.
Ipo miradi midogo ambayo imetekelezwa na tumeona , ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, mfano barabara ya Msata-Bagamoyo na Kagoma-Biharamuro-Lusahunga na mabadiliko kwenye sekta ya afya ambayo yamekua msaada mkubwa katika kubadilisha maisha ya watanzania na kuifanikisha safari ya nchi kuelekea uchumi wa kati na ujenzi wa Tanzania ya viwanda.
Kama Serikali iliahidi na imetekeleza, yatupasa kuhakikisha tunafanya kazi kwa biidi kwenye miradi hiyo na kuhakisha tunailinda ili isiharibike kwa namna yoyote badala ya kutoa pongezi za maneno matupu.
No comments:
Post a Comment