Balozi maalum wa DStv na Mwanariadha pekee
wa Tanzania liyeshiriki mashindano ya London Marathon Alphonce Simbu amerejea
nyumbani na kutoa onyo kali kwa wale atakaokabiliana nao kwenye mashindano
yajayo ya dunia yatakayofanyika mwezi Agosti jijini London.
Simbu ambaye alishika nafasi ya tano katika
mashindano hayo na kujishindia kitita cha dola za marekani 10,000 aliwasili
katika uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro na kulakiwa na maafisa
mbalimbali akiwemo Meneja Uhusiano wa Multichoice Tanzania Johnson Mshana,
Meneja wa mwanariadha huyo Francis John.
Akizungumza katika mkutano na
waandishi wa habari uliofanyika jijini Arusha muda mfupi baada ya yeye kuwasili
Simbu aliwashukuru sana watanzania wote kwa moyo wao na jinsi walivyomuunga
mkono na kumtakia kila la heri katika mashindano hayo. Amesema alifarijika sana
na pia kupata moyo zaidi alipokuwa akipokea salamu kutoka kwa watanzania kote
ndani nan je ya nchi.
Akizungumzia mashindano hayo,
Simbu amesema yalikuwa na changamoto kama yalivyo mashindano mengine makubwa ya
kimataifa kwani yalishirikisha vigogo ambao wengi wao wana uzoefu mkubwa katika
mashindano mbalimbali na wengine pia ni washindi wa mashindano ya hapo awali.
Mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho
Gambo ambaye aliwakilishwa na mkuu wa Wilaya ya Monduli Idd Kimanta alisema
mkoa mzima wa arusha umepokea kwa Furaha habari za mkazi wao kufanya vizuri
katika mashindano makubwa kama hayo na kwamba wataendelea kushirikiana na Simbu
na kumsaidia kwa kadiri itakavyowezekana ili kumuwezesha kuendelea kuuwakilisha
vizuri mkoa na taifa kwa ujumla kwenye michuano ya kimataifa.
Amesema kuwa ushindi wa simbu
uwe ni chachu kwa vijana wengine wa kitanzania wenye vipaji na wasibaki nyuma
bali wajitokeze na watie nguvu katika kuonyesha vipaji vyao. “Tuna vipaji vingi
sana tena siyo kwa riadha tu, bali vya kila aina, cha mshingi ni kushirikiana
kwa karibu na wadau ili kuhakikisha vipaji hivyo vinaibuliwa na kuendelezwa kwa
manufaa ya taifa kwa ujumla” alisema mkuu huyo wa mkoa.
Naye Meneja Uhusiano wa
Multichoice Tanzania Johnson Mshana amesema wao kama wadhamini wa Simbu
wamepokea kwa Furaha kubwa matokeo hayo ambayo yanaonyesha kuimarika kwa
kiwango cha Simbu. “Tuliamua kumdhamini Simbu tukiamini kabisa kuwa atakuwa
nyota na atailetea Tanzania sifa. Tuna dhamira kubwa nay a dhati kabisa ya
kuhakikisha kuwa siku moja wmbo wetu wa taifa unapigwa katika mashindano ya
Olimpiki. Bila shaka hili lipo karibu kutokea”.alisema Mshana.
Multichoice Tanzania inamdhamini
Simbu kwa muda wa mwaka mzima kwa lengo la kufanikisha maandalizi yake ya
kushiriki katika mashindano ya Dunia ya mwaka huu. Udhamini huu ulianza tangu
mwaka 2016 ambapo Multichoice humpatia Alphonce posho ya kujikimu pamoja na
kusaidia kambi yake ya mazoezi.
Alphonce, ambaye ni
Mtanzania wa kwanza kushinda medali ya dhahabu katika mashindano maarufu ya
Standard Chartered Mumbai Marathon, anatarajiwa kushiriki mashindano ya riadha
ya dunia yatakayofanyika London mnamo mwezo Agosti mwaka huu.
Balozi maalum wa DStv na Mwanariadha pekee
wa Tanzania liyeshiriki mashindano ya London Marathon Alphonce Simbu akiwa na baadhi ya maafisa wa Multichoice Tanzania.
Balozi maalum wa DStv na Mwanariadha pekee
wa Tanzania liyeshiriki mashindano ya London Marathon Alphonce Simbu akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Monduli Idd Kimanta
Balozi maalum wa DStv na Mwanariadha pekee
wa Tanzania liyeshiriki mashindano ya London Marathon Alphonce Simbu akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani)
No comments:
Post a Comment